KiturukiMakala hii inahusu lugha ya Kituruki. Kwa familia yake ya lugha, angalia, tazama Lugha za Kiturki.
Kituruki (jina asili: Türkçe; kwa Kiingereza:Turkish) ni lugha rasmi nchini Uturuki. Ni lugha yenye wasemaji milioni 80. Hivyo ni lugha yenye wasemaji wengi zaidi kati ya Lugha za Kiturki zinazozungumzwa na watu milioni 170 katika Asia ya Magharibi na Asia ya Kati. Kuna wasemaji nchini Uturuki, kwenye kisiwa cha Kupro, Bulgaria, Ugiriki, Masedonia na katika nchi kadhaa zilizokuwa sehemu za Dola la Uturuki. Kutokana na uhamiaji wa Waturuki kuna pia wasemaji milioni kadhaa katika nchi za Umoja wa Ulaya. Kituruki cha Uturuki ni lugha kubwa katika kundi la lugha zinazofanana zinazoitwa "Kiturki" (ing. Turkic). Hivyo wasemaji wa Kituruki huelewana kwa kiasi kikubwa na wasemaji wa Kiazeri, Kiturkmen na Kiqashgai. Wasemaji wa lugha za Kiturki waliingia katika eneo la Uturuki ya leo tangu mwaka 1000. Wakati wa Dola la Uturuki lugha yao ilikuwa lugha ya utawala na fasihi andishi. Hadi Atatürk Kituruki kile kilitumia maneno mengi ya Kiarabu na Kiajemi kikaandikwa pia kwa Alfabeti ya Kiarabu. Tangu mwaka 1923 lugha imeandikwa kwa alfabeti ya Kilatini na maneno yenye asili ndani ya Kituruki yalitafutwa. Viungo vya nje
|