SayariSayari (kwa Kiingereza planet) ni kiolwa kikubwa cha angani kinachozunguka jua (au nyota nyingine) na kung'aa kutokana na nuru ya jua iliyoakisiwa, tofauti na nyota na jua zinazong'aa peke yake. Kwa macho inaonekana kama nyota, lakini baada ya kuitazama kwa muda wa mwaka inaonekana inabadilisha mahali pake angani, tofauti na nyota kwa jumla. Tofauti kubwa kati ya sayari na nyota ni kwamba, nyota ukiitazama inametameta ila sayari haiwezi. JinaJina la Kiswahili "sayari" lina asili yake katika neno la Kiarabu كوكب سيار kaukab sayar "nyota inayosogea" [1]. Neno hilo la Kiarabu linalingana au ni tafsiri ya neno la Kigiriki πλανήτης planetes (lenye maana ya "yenye kusogea") ambalo ni asili ya jina "planet" kwa Kiingereza na lugha nyingine za Ulaya. Tangu zamani watazamaji wa anga katika tamaduni mbalimbali walitambua ya kwamba nyota kwa kawaida hukaa mahali pamoja lakini nyota chache zinabadilisha polepole mahali pake kati ya nyota nyingine zikifuata njia zinazorudia kila mwaka. Nyota hizo ziliitwa "nyota zinazosogea". Ufafanuzi wa sayariZamani kulikuwa na sayari 5 tu zilizoonekana angani kwa macho matupu kama nyota zinazobadilisha mahali[2]. Tangu kupatikana kwa mitambo kama darubini miaka 400 iliyopita idadi ya violwa angani vyenye miendo ya pekee imeongezeka sana lakini imeonekana pia kuna tofauti kubwa sana kati ya violwa hivi. Hivyo wataalamu wa Umoja wa kimataifa wa astronomia (IAU) walikubaliana mwaka 2006 kuhusu ufafanuzi wa sayari. Kiolwa cha angani kinahesabiwa kuwa sayari kama kinatimiza masharti matatu:[3]
Ufafanuzi huo uliamuliwa kwa kura hata kama wanaastronomia wengine hawakukubali. Azimio hili liliondoa hadhi ya sayari kwa Pluto [4] iliyowahi kutazamwa kuwa sayari katika miaka iliyopita. Wakati mwingine kuna violwa vingine ambavyo vinavyoitwa pia "sayari" ingawa havitoshelezi masharti yote matatu.
Majina ya sayariKwa Kiswahili kuna tofauti kuhusu majina ya sayari kati ya vikundi viwili:
Sayari za jua letuJua letu lina sayari nane ambazo ni Utaridi (Mercury), Zuhura (pia: Ng'andu; Venus), Dunia yetu (Earth), Mirihi (Mars), Mshtarii (Jupiter), Zohali (Saturn), Uranusi na Neptuni. Toka mwaka 1930 hadi Agosti 2006 Pluto ilikuwa ikitambulika kama sayari hivyo kufanya idadi ya sayari zinazojulikana kuwa tisa. Hata hivyo chama chenye mamlaka juu ya masuala ya sayari na nyota, Umoja wa Kimataifa wa Astronomia kimetangaza rasmi kuwa Pluto si sayari na kuiita sayari kibete[7]. Vitabu vingi vya shule vimebadilishwa kulingana na uamuzi huo, japo bado kuna vitabu ambavyo bado vinaonyesha Pluto kuwa sayari kweli. Sayari tano za Utaridi, Zuhura, Mirihi, Mshtarii na Zohari [8] huonekana kwa macho kama nyota angani. Lakini tangu zamani zilitambuliwa kuwa tofauti kwa sababu hazikai mahali palepale kama nyota ya kawaida bali huhamahama angani. Kutokana na tabia hii zimetazamwa mara nyingi kuwa na nguvu za pekee au hata kuwa miungu. Unajimu umetumia mwendo wa sayari zinazoonekana kwa macho kama msingi muhimu wa makadirio yao. Sayari nyingine katika mfumo wa jua zimetambuliwa tangu kutokea kwa astronomia ya kisayansi kwa darubini. Hizi ni Uranus na Neptun. Katika lugha ya Kiswahili sayari zinazoonekana kwa macho huwa na majina ya asili ya Kiarabu isipokuwa Zuhura ina jina la Kibantu la Ng'andu pamoja na jina la asili ya Kiarabu. Majina mengine ni ya asili ya Kilatini. Jumla ya jua, sayari zote 8 pamoja na miezi yao, sayari kibete, vimondo, nyotamkia na asteroidi inaitwa mfumo wa jua. Aina za sayariSayari za jua letu hutofautiana kwa ukubwa na muundo. Mshtarii (Jupiter) ni sayari kubwa na masi yake ni mara 318 masi ya dunia yetu. Sayari ndogo ni Utaridi na masi yake ni takriban nusu ya dunia. Kutokana na umbali tunatofautisha "sayari za ndani" kuanzia Utaridi (Mercury) hadi ukanda wa asteroidi, halafu "sayari za nje" kuanzia Mshtarii (Jupiter) hadi Uranus. Muundo wa sayari ni tofauti; kuna vikundi kulingana na mata inayojenga sayari:
Sayari nje ya mfumo wa jua letuWataalamu wa astronomia wamegundua sayari-nje (ing. exoplanets) yaani sayari zilizoko nje ya mfumo wa Jua letu zinazozunguka nyota mbalimbali. Kutokana na umbali mkubwa na matatizo ya utazamaji kwa muda mrefu hakukuwa na uhakika kama nyota kuwa na sayari ni jambo la kawaida angani au kama sayari ni chache tu. Tangu 1995 kuwepo kwa sayari-nje kuliweza kukadiriwa kutokana na mabadiliko ya mwendo wa nyota kadhaa yaliyoweza kuelezwa tu kutokana na masi ya karibu inayobadilisha mwendo wa kawaida. Baada ya kuboreshwa kwa vifaa vipimo vya mabadiliko ya mng'aro vimeonyesha mipito ya sayari, maana wakati wa kupita kwa sayari kati ya nyota fulani na mtazamaji duniani sayari inafunika sehemu ya nyota yake, hivyo mng'aro wake unapungua. Kiasi cha mabadiliko ya mng'aro kinaruhusu kukadiria umbali wa sayari na nyota yake na ukubwa wake. Sayari-nje nyingi zimetambuliwa kwa kutumia mbinu huu. Kutokana na maendeleo ya darubini imewezekana tangu mwaka 2004 kutambua sayari-nje kadhaa moja kwa moja lakini idadi yao hadi sasa ni ndogo wa sababu ugunduzi ni vigumu. Hadi Aprili 2019 kuwepo kwa sayari-nje 4,048 kumethibitishwa na kati ya hizi mifumo ya sayari 659 imetambuliwa ambako kuna zaidi ya sayari moja.[9] Nyingi kati ya hizo zilikuwa na ukubwa kufanana na Mshtarii au kubwa zaidi. Lakini sayari ndogo zaidi zimetambuliwa pia. [10] Marejeo
Viungo vya nje
|