Roma ya KaleRoma ya Kale ni ustaarabu uliokua kutoka katika mji Roma, ulioanzishwa katika rasi ya Italia kabla ya karne ya 9 KK. Katika kipindi cha karne kumi na mbili cha uhai wake, ustaarabu wa Roma ulibadilika toka kuwa dola-mji, kwanza ufalme halafu jamhuri ya Roma yenye athira katika Italia, na hadi kuwa milki kubwa. Roma ya Kale ilikuja kutawala Ulaya Magharibi na eneo zima linalozunguka bahari ya Mediteranea kwa njia ya vita au kwa njia ya maungano na maeneo. Baada ya karne za upanuzi uhamiaji wa mataifa mapya ya Wagermanik pamoja na mashambulio kutoka Asia zilisababisha hatimaye kuanguka kwa Dola la Roma kuanzia karne ya 5 BK. Sehemu ya magharibi ya milki dola liliporomoka kabisa likiendelea na umoja wa kiutamaduni lililotunzwa hasa na Kanisa Katoliki chini ya uongozi wa Papa wa Roma. Sehemu ya mashariki ya Dola iliyoongozwa kutoka Konstantinopoli iliendelea. Tabia yake ilibadilika polepole kuwa milki ya Wagiriki ikaitwa baadaye Milki ya Byzanti ikiendelea hadi mwaka 1453, Waturuki walipotwaa mji wa Konstantinopoli na kuimaliza.
|